ADVERTISE WITH US HERE FOR YOUR OWN EXPANSION AND PROSPERITY

.
.

Tuesday, December 6, 2011

Nchi za Marekani na Uchina Zachangamkia Kiswahili

UKISIKILIZA watu kutoka nje ya Tanzania wanavyozungumzia nafasi ya Kiswahili kwenye ulingo wa kimataifa, utakubaliana moja kwa moja na usemi kuwa  nabii hakubaliki kwao.

Wakati kukiwa na idadi kubwa ya  raia wa kigeni wanaokuja nchini  kujifunza lugha ya Kiswahili, bado Watanzania hawaithamini lugha yao kiasi kwamba mpaka sasa hawajaona umuhimu wa kuitumia lugha hiyo kufundishia katika madaraja yote ya elimu.
Baadhi ya wanafunzi kutoka mabara ya Asia na Amerika  wanaosoma Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,   wanaeleza sababu zilizowasukuma kuja kusoma Kiswahili na nafasi ya lugha hiyo kimataifa.Wanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Tianjin cha nchini  China, wanasema wamechagua kusoma Kiswahili kwa sababu wanajua kwa siku za usoni kitakuja kuwa moja ya lugha kubwa duniani.

Wanafunzi hao  wanasema  kwa kipindi cha miaka miwili walikuwa wakijifunza lugha hiyo kupitia walimu kutoka Zanzibar na China.Wang Panlolei  ambaye baada ya kufika nchini,  mwalimu wake alimpa jina la Aisha kutokana na kushindwa kutaja jina lake la asili, anasema ameamua kujifunza Kiswahili kwa sababu Tanzania ni moja ya nchi zinazoendelea kama ilivyo China.

“Nilipotakiwa kuchagua lugha nitakayosoma,  niliingia kwenye mtandao ndiyo nikaona Kiswahili, Nikaona  ni lugha inayozungumzwa na watu wa Afrika Mashariki na nilipenda utamaduni wa watu hawa. Kutokana na hali hiyo nikaamua kusoma Kiswahili,” anasema na kuongeza:
“Nilikuwa nafuatilia sana habari za Kiswahili kwenye mtandao na katika kutafuta habari,  niliona mpaka gazeti la Mwananchi na wakati mwingine nikawa nalitumia kupata habari za Kiswahili.”

Anaeleza kuwa  mbali na gazeti hili, pia hutumia Redio za BBC na Kiswahili China Radio International kujifunza lugha ya Kiswahili.Hata hivyo anasema kuwa Kiswahili alichojifunza kwa miaka miwili nchini China ni tofauti na kile wanachokitumia  Watanzania hasa katika mazungumzo.


“Kule sisi tunajifunza sana sarufi na pia hatupati nafasi kubwa ya kuzungumza Kiswahili…, ukisoma kwenye kitabu unaambiwa ukitaka kumsalimia mtu unamwambia ‘hujambo’, lakini ukija huku watu wanasalimiana ‘mambo, ’” anasema mwanafunzi huyo.Kuhusu nafasi ya Kiswahili kimataifa, anasema  hakuna ubishi kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya Kiafrika.

“Kiswahili ni lugha ya kipekee,  ina nafasi sana ya kuwa lugha kubwa kama zilivyo nyingine duniani, lakini bado inatakiwa kipewe nafasi kubwa kama kufundishia shule za sekondari, vyuoni na pia kitangazwe zaidi,” anaeleza.
Naye Wu Zhen Huan ama Bakari kama anavyojulikana kwa walimu wake, anasema aliijua lugha ya Kiswahili kupitia mtandao baada ya  kuvutiwa na utamaduni wa watu wake.

“Lugha ni sehemu kubwa ya utamaduni wa mtu, kwa hiyo najua mpaka nikihitimu shahada yangu ya Kiswahili nitakuwa nimeijua sehemu kubwa ya utamaduni wa Watanzania,” anasema.

Anasema ili kuendeleza utamaduni wa Kitanzania, Serikali haina budi kuongeza juhudi za kuitangaza lugha ya Kiswahili na kuitumia kama lugha ya kufundishia katika elimu kama ilivyo China.

Kwa upande wake,  Ye Tianfa au Suleiman  anasema ni Watanzania wenyewe watakao weza kukiinua Kiswahili kwa kukipenda na kukithamini.Pia Yu Shaoshuai ama Hamisi, anasema aliamua kujifunza Kiswahili baada ya kushindwa kuelewana na wafanyabiashara wengi kutoka Afrika Mashariki wanaokwenda kununua bidhaa katika mji wa Yiwu mji ambao ndiko anakotoka.

“Nikimaliza shahada  yangu ya Kiswahili, nitafanya biashara vizuri kwa sababu nitakuwa sisumbuliwi tena na lugha hii,” anasema Shaoshuai.Naye  Zhu Chanjiao anayeitwa pia kwa jina la Lulu, anasema sababu kubwa ya kujifunza Kiswahili ni kutokana na kiu yake ya kueneza utamaduni wa Kichina katika nchi za Afrika Mashariki.

“Nikimaliza chuo najua nitakuwa na nafasi nzuri ya kueneza utamaduni wetu wa China Afrika Mashariki kwa sababu lugha itakuwa hainisumbui,” anabainisha.

Wanafunzi hao wanaosoma kwa  ufadhili wa pamoja wa Serikali za China na Tanzania, watatumia muda wa miezi nane kujifunza Kiswahili kabla ya kurejea kwao kumaliza masomo yao.

Mwanafunzi mwingine,  Chris Vavdo kutoka Marekani, anasema japo kwa sasa Kiswahili hakina nafasi  katika  kimataifa kikilinganishwa na lugha kama Kiingereza, au Kifaransa, anatoa rai kwa Watanzania kuanza kukipandisha chati kwa kuitumia kama lugha kuu katika elimu.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili ya chuo hicho(Tataki), idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nje ya nchi wanaosoma Kiswahili kwenye taasisi hiyo, wanatoka nchi za China na Marekani.

Tataki inasema ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine vya nje, ni moja ya sababu inayoongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma Kiswahili katika taasisi hiyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anasema  sera ya elimu inayoendelea kuandaliwa, italeta mabadiliko mbalimbali katika elimu ikiwamo kukipa hadhi Kiswahili

Akifafanua anasema  katika mabadiliko hayo, lugha ya kufundishia katika madaraja ya sekondari na msingi itakuwa Kiswahili na Kiingereza tofauti na sasa ambapo kwa upande wa sekondari lugha inayotumika ni  Kiingereza pekee.
Kwa mujibu wa Dk Kawambwa,  shule za awali zitatumia Kiswahili huku vyuo vya ualimu  vikitumia  Kiswahili na Kiingereza. “Shule nyingine zitatumia Kiingereza na nyingine zitaruhusiwa kutumia Kiswahili kwa upande wa sekondari,” anasema
Na Mwananchi
Posted By MgonjahMedias Team Edited by AmanyMei-Xing Zachariéliz
Follow us on Facebook

0 comments:

Post a Comment

Subscribe